toniking toniking Author
Title: Majaliwa acharuka
Author: toniking
Rating 5 of 5 Des:
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Evarist Ndikilo kuziandikia barua taasisi za serikali, umma na binafsi...

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kuziandikia barua taasisi za serikali, umma na binafsi zenye viwanja visivyoendelezwa mjini hapa, wajieleze ni lini wataanza kuviendeleza na ndani ya wiki mbili watoe majibu, vinginevyo viwanja hivyo vitanyang’anywa.
Agizo hilo alilitoa jana mjini hapa wakati akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015 - 2020) na Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, mkoani Pwani.
Kabla ya agizo hilo la Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa huo, Ndikilo alishitaki kwa Waziri Mkuu taasisi za umma na binafsi, ambazo zimehodhi viwanja kwa muda mrefu kati ya miaka mitano hadi kumi bila kuviendeleza na kumuomba (Majaliwa) afanye uamuzi kwa sababu wapo watu wanavihitaji.
“Kibaha ni kimbilio la mkoa wa Dar es Salaam, kule kumejaa na hapa kuna nafasi kwa hiyo hawa ambao hawajaendeleza, waandikie barua leo hii na uwape wiki mbili waeleze ni lini watakuwa tayari kuanza kazi hiyo,” aliagiza Majaliwa.
Waziri Mkuu alizitaja taasisi hizo ambazo hazijaendeleza viwanja kuwa ni pamoja na Hazina Ndogo yenye viwanja viwili na kimoja chenye namba 232 kimeendelezwa, lakini kingine namba 221 hakijaendelezwa.
Taasisi nyingine na viwanja vyao kwenye mabano ni Chuo Kikuu Huria (OUT) (kitalu na. 228), Njuweni Institute (kitalu na. 229), Shirika la Umeme (Tanesco) (kitalu na. 218), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (kitalu na. 233), Kampuni ya SF Group (kitalu na. 225), Benki ya CRDB na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru).
Alimtaka Ndikilo kuwaandikia barua na na zijibiwe ndani ya wiki mbili.
“Najua kuna watu wa Serikali watasema hawana bajeti, lakini Bunge la Bajeti linaanza Aprili mwakani, kwa hiyo wajipange kwenye bajeti ijayo, ili ifikapo Julai mosi, 2018 kama hawajaendeleza, tuwachukulie hatua, tutachukua viwanja vyetu tuwape wengine na hawa wanaosusa watakapokuwa tayari waombe upya”, alisema Majaliwa.
Awali, akizindua mradi huo, Majaliwa alisema wananchi wengi wanapata shida ya kufikia huduma mbalimbali za kijamii, zikiwemo za mahakama katika ngazi ya kata na wilaya, jambo ambalo halikubaliki.
“Nichukue fursa hii kuwakumbusha wenzetu wa mahakama kuwa, sisi sote tupo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania, hivyo mipango na mikakati yetu iangalie utaratibu utakaotoa haki kwao ili kuwaongezea imani kwa Mahakama na Serikali kwa ujumla,” alisema Waziri Majaliwa.
Alisema mpango mkakati uliozinduliwa jana ni dalili nzuri ya uongozi na utendaji wa mahakama ambayo inajitambua, inayojua inakwenda wapi na kwa muda upi na kuweka utaratibu wa kujipima na kujitathmini kwa kila hatua.
Mpango mkakati huo wa mahakama, utakaogharimu Sh bilioni 139.5 (sawa na dola za Marekani milioni 65), utagharimiwa kwa fedha kutoka katika bajeti ya Serikali na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyohudhuria uzinduzi huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande alisema mahakama imeanzisha kada mpya ya watumishi wa kusimamia masuala ya fedha ili kada ya sheria iendelee na shughuli za mahakama tu.
Alisema kuzinduliwa kwa mpango mkakati wa mwaka 2015/16 hadi 2019/20 pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania, kutaiwezesha mahakama kujenga mahakama ya Hakimu Mkazi kati ya tano hadi nane, mahakama za wilaya 30 hadi 40 zikitegemezwa kujengwa na za Mwanzo 70 hadi 100 zitajengwa ndani ya miaka mitano ya mpango huo.
Jaji Chande alisema kati ya mikoa 26 nchini, ni mikoa 14 tu ambayo ina Mahakama Kuu. Alisema kwamba mahakama hizo zinaweza kujengwa kwenye mikoa ya Njombe, Geita, Simiyu, Katavi, Singida, Manyara, Songwe, Lindi, Pwani na Morogoro.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top