Unknown Unknown Author
Title: Simba yaendeleza ufalme kwa kuichapa 1-0 Mbao FC
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Simba tangu ilazimishwe sare ya bao 1-1 na Watani zao Yanga Oktoba 1 kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaa...
Ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Simba tangu ilazimishwe sare ya bao 1-1 na Watani zao Yanga Oktoba 1 kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam
Bao la dakika ya 86 lililofungwa na kiungo Mzamiru Yasini liliendelea kumweka Simba katika wakati mzuri wa kuongoza dhidi ya Mbao FC na kuifanya timu hiyo kuendelea kubaki kileleni ikifikisha pointi 26 katika michezo 10 ya ligi ya Vodacom waliyocheza hadi sasa.

Simba iliwalazimu kupambana vilivyo kupata ushindi huo ambao ulishapotea katika fikra za mashabiki wengi wa timu hiyo licha ya kwamba kabla ya mchezo huo wenyeji Simba walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya ushindi tena kwa idadi kubwa ya mabao kutokana na udhaifu wa timu wanayokutana nayo.

Mbao FC, ilionyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo na kuwabana vilivyo wenyeji wao Simba na kushuhudia washambuliaji Laudit Mavugo Ibrahim Ajibu na Shizza Kichuya wakishindwa kuipenya ngome yao iliyokuwa chini ya ulinzi wa beki Asante Kwasi.

Katika dakika ya sita Kichuya alipata nafasi nzuri lakini shuti alilopiga lilipaa juu ya lango la Mbao FC, ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza ligi ya Vodacom msimu huu.

Simba waliendelea kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Mbao FC na Mavugo aliyerejeshwa kwenye kikosi cha kwanza na alipata nafasi nzuri lakini alishindwa kumalizia krosi ya Janvier Bukungu na kipa wa Mbao Emmanuel Mseja kuupangua mpira huo kuwa kona.

Kiungo na nahodha wa Simba Jonas Mkude angeweza kuifungia bao Simba dakika ya 28 baada ya kupiga shuti lakini mpira huo ulimgonga beki Steven Kigocha na mpira kutoka nje na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Baada ya kupita dakika 25 Mbao walionekana kuzinduka na kuanza kupanga mashambulizi yao huku wakimtumia mshambuliaji mmoja Salum Sued, ambaye alionyesha kuwasumbua walinzi wa Simba Method Mwanjali na Juuko Murshid.

Katika dakika ya 39 Sued alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini akiwa amebaki na kipa mshika kibendera Michael Mkongwa, alinyanyua kibendera chake juu akimaanisha mchezaji huyo ameotea na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa sare.

Kipindi cha pili Simba walionekana kukianza kwa kasi huku wakifanya mashambulizi mengi kwenye lango la Mbao na kufanikiwa kupata kona tatu za haraka lakini walishindwa kuzitumia.

Ajibu alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao la kuongoza timu yake dakika ya 49 kufuatia makosa ya kipa wa Mbao FC, Mseja, lakini mpira wake uliokolewa vizuri na beki Steven Mganya.

Baada ya kuona mambo magumu kocha Omog wa Simba alimtoa Mavugo na Ajibu na nafasi zao kuchukuliwa na Fredrick Blagnon na Mohamed Ibrahim ambao waliendelea kuliza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Mbao lakini kwa nyakati tofauti wachezaji hao nao walionekana kupoteza nafasi walizozipata.

Blagnon aliifungia Simba dakika ya 56, lakini mwamuzi Hance Mabena alilikata bao hilo kutokana na mchezaji huyo kuushika mpira kabla hajafunga.

Mchezo huo uliendelea kuwa wa upinzani kwa timu zote kushambuliana na kusababisha hatari kila upande lakini hasa wageni Mbao waliokuwa wakifanya mashambulizi ya kustukiza lakini bado mambo yalikuwa magumu.

Kocha wa Mbao Ettiene Ndaliyejige,alimtoa mshambuliaji Huseni Sued dakika ya 76 na kumuingiza Frank Damas ambaye hakuwa na madhara kwa mabeki wa Simba na kufanya mashambulizi kupungua kwenye lango lao.

Timu zote ziliendelea kushambuliana zikitafuta pointi tatu lakini wakati mashabiki wakiamini mpambano huo utamalizika kwa sare Mzamiru Yasin aliwanyanyua vitini mashabiki wa timu yake baada ya kufunga bao jepesi kufuatia pasi nzuri ya Blagnon.

Huo unakuwa ushindi wa tatu mfululizo kwa Simba tangu ilazimishwe sare ya bao 1-1 na Watani zao Yanga Oktoba 1 kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top