toniking toniking Author
Title: Nchi 26 zaapa kukabili ukatili dhidi ya albino
Author: toniking
Rating 5 of 5 Des:
HIVI karibuni, watu wapatao 150 kutoka nchi 26 za Afrika, wameshiriki mkutano wa ushauri ukilenga kuweka mikakati kuhusu watu wenye ualbino...
HIVI karibuni, watu wapatao 150 kutoka nchi 26 za Afrika, wameshiriki mkutano wa ushauri ukilenga kuweka mikakati kuhusu watu wenye ualbino.

Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, umewezesha washiriki kuainisha hatua za kufanikisha lengo hilo. Washiriki hao ni kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali, taasisi za haki za binadamu za kitaifa, kikanda na hata kimataifa. Taarifa zinaonesha takribani matukio 450 ya uvamizi wa watu wenye ualbino, yameripotiwa katika nchi 25 za Afrika. Inaelezwa kuwa matukio mengi ni ya kuanzia mwaka 2006. Hata hivyo, taarifa zinasema matukio mengi hayaripotiwi kutokana na siri iliyopo juu ya masuala ya ushirikina.
Licha ya watu wenye ualbino kustahili haki zote ikiwemo ya kuishi, mashambulio haya yaliyojikita katika imani za kishirikina, yamesababisha vifo vyao na wengine kubaki na ulemavu wa kudumu. Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez, katika mkutano huo, anaelezea umuhimu wa usawa, heshima, utu na haki kwa watu wote. Anataja Malengo ya Maendeleo Endelevu yatafikiwa, ikiwa ni pamoja na kuzingatia suala zima la haki ya watu wenye ualbino.
Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu), Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk Abdallah Possi anasisitiza juu ya hilo akisema, maendeleo endelevu yatatimia endapo kila mtu atahusishwa. Dk Possi anasema maendeleo endelevu yanapaswa yaende bega kwa bega na usawa, heshima na haki kwa kila mtu. Anawahakikishia washiriki wa mkutano huo namna ambavyo serikali imejizatiti kufanikisha hilo.
Ubia wa serikali na sekta binafsi unatajwa kuwa ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo la kupambana na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino kama ambavyo nchi imefanikiwa katika kupambana na Ukimwi. Anataja hatua ambazo Tanzania imezichukua ni pamoja na kukusanya kanzi data ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wakati huo huo kuripoti matukio hayo kwenye vyombo vya habari kwa mtazamo chanya. Vile vile anasema kumeanzishwa mkakati wa kuratibu na kufuatilia kuhakikisha utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu (CRPD).
Dk Possi anasema ukatili kwa watu wenye ualbino unaweza ukawa wa kimwili au wa kisaikolojia. Anasema umekuwa ama ukawa wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja. Anasisitiza kuwa haki ya kulindwa dhidi ya ukatili, imeainishwa kwenye misingi ya kimataifa ya haki za binadamu na hata kwenye sheria za nchi. “Hatua za muda mfupi, kama vile kuwafikisha mahakamani wahusika zinaweza zisikabili mzizi wa tatizo,” anasema Possi.
Dk Possi anataja hatua za muda mrefu ni pamoja na kutoa elimu na huduma za kiafya kwa wenye ulbino huo. Anataja changamoto zilizopo, ni pamoja na matumizi ya vituo kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa ngozi ambayo kimsingi, husababisha kuwatenga na familia zao na jamii kwa ujumla. Nemes Temba kutoka Chama cha Albino Tanzania anahimiza umuhimu wa kufanyia kazi suala zima la afya kwa watu wenye ulbino huo.
Pia anasisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuhamasisha uelewa kuhusu ulemavu huo kwa taarifa zenye mrengo chanya. Licha ya Tanzania, nchi nyingine washiriki wa mkutano sanjari na taasisi mbalimbali, wanaweka bayana namna ambavyo hawako nyuma katika kukabili ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi. Mathalani, Kenya kupitia kwa mbunge Issaac Nwaura, anaeleza mikakati hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa Chama cha Wenye ulemavu Ualbino mwaka 2006.
Anasema nchini mwake wanayo programu ambayo imewezesha ufadhili wa elimu kwa watoto zaidi ya 40 sanjari na kutoa huduma za tiba ya macho, kuwapa mavazi maalumu na kuendelea kufanya ushawishi juu ya haki zao. Umeanzishwa mkakati wa dharura wa kusaidia waathirika wa uvamizi, lakini pia kutoa msaada wa kisheria kwa kesi zinazohusu albino. Mbunge huyo anahimiza umuhimu wa kuhusisha vyombo vya habari kuhakikisha vinatoa taarifa chanya zinazohusu watu wenye ulemavu wa ngozi.
“Ingawa wajibu wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanafurahi haki zao za binadamu unaegemea kwa serikali, ubia na vyama vya kijamii pia ni suala muhimu,” anasema Nwaura. Mwakilishi kutoka Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu la Kenya, Alex Munyere, anahimiza umuhimu wa kuwa na mtu maalumu ndani ya baraza kushughulikia masuala ya watu wenye ualbino.
Kwa upande wake, Bernard Mogesa, kutoka Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya, anasema jukumu la tume ni kufuatilia namna ambavyo nchi inakidhi maelekezo ya kimataifa na kikanda katika kujenga ubia wa kufanikisha haki za watu hao wenye ualbino. Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Under the Same Sun (UTSS), Vicky Ntetema, anaelezea nafasi yao katika kukabili ukatili kwa wenye ualbino.
Anataja mpango wa elimu unaotekelezwa, ambao shirika limetoa ufadhili kwa takribani watu 300 wenye ualbino kuanzia ngazi ya chekechea hadi kiwango cha Shahada ya Uzamivu. Anahimiza umuhimu wa watoto wenye ualbino kupatiwa elimu ili wawe kivutio na mfano kwa wengine (wasio na ulemavu). “UTSS imeanzisha mwongozo kwa walimu, watoa huduma na wazazi juu ya namna ya kuwatunza na kuwafundisha watoto wenye ulemavu wa ngozi,” anasema Ntetema.
Vile vile Ntetema anasema shirika limejitengenezea timu ambayo hutoa huduma ya haraka kwa waathirika wa mashambulizi sanjari na kukusanya taarifa kwa kufanya kazi karibu na jamii. Ntetema anasisitiza umuhimu wa kupitia upya baadhi ya sheria ikiwemo Sheria ya Uchawi ya mwaka 1928 na Sheria ya Tiba Asilia na Dawa mbadala (za Tanzania).
Kwa mujibu wa mwakilishi huyu wa shirika, sheria hizo zimekuwa zikileta ugumu katika upelelezi kutokana na kuruhusu matumizi ya sehemu ya viungo vya wanyama katika tiba ingawa sheria inazuia kumiliki viungo vya binadamu isipokuwa kwa madaktari. Kwa ujumla, maoni ya wachangiaji wengi, yanasisitiza umuhimu wa kupeleleza na kushitaki usilenge tu wanaofanya mashambulio, bali pia watu wanaowatuma watafute viungo hivyo kwa kuwalipa fedha.
Pia wanahimiza kukemea ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya kundi hili kwa kuwawezesha kupata huduma za afya, kupata elimu na ajira bila kubaguliwa. Kupitia mkutano huo, kila nchi/taasisi (washiriki), zimejitia ‘kitanzi’ cha kukabili adha na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino huku nyingi zikiahidi kufanyia kazi suala zima la sheria. Mathalani, Namibia imeahidi kuanzisha Sheria ya Ulemavu na wakati huo huo kuelimisha wadau mbalimbali wakiwemo wabunge, juu ya haki za watu wenye ualbino.
Malawi pia inasema itafanya marekebisho kwenye sheria zilizopo, ikiwa ni pamoja na kurekebisha vipengele kuwezesha mashitaka dhidi ya wanaofanya ukatili. Eneo lingine ambalo nchi zimeahidi kufanyia kazi, ni kuelimisha wadau mbalimbali, hususani mahakimu na waandishi wa habari, namna ya kushughulikia kesi na masuala ya wenye ulemavu wa ngozi. Malawi kupitia Wizara ya Jinsia na Ulemavu, imesisitiza juu ya hilo.
Afrika Kusini pia pamoja na kuahidi kutoa usaidizi mkubwa wa kisheria, itaandaa mkutano mkubwa wa watu wenye ualbino. Ahadi ya Kenya ni kuhakikisha katika sensa za watu zijazo, watu wenye ualbino wanaingizwa. Vile vile itatoa kipaumbele katika kuelekeza rasilimali kwa kundi hilo. Msumbiji pia inaweka bayana kujikita katika kutoa uelewa na wakati huo huo kutafiti zaidi sababu za kuvamiwa kwa albino.
Tanzania pia inasema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika vita dhidi ya mauaji ya albino. Mathalani, Tanganyika Law Society inaahidi kutoa mafunzo kwa mawakili kuhusu Sheria ya DNA. Kwa upande wake, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania, kinaahidi kufuatilia bajeti kuhusu masuala ya jinsia hasa kuhusu watu wenye ualbino. Shirika la Under the Same Sun linaahidi kuendelea kufanya kazi na jamii katika kukusanya taarifa juu ya watu wenye ualbino.
Mkutano huo ulioandaliwa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulemavu wa ngozi, ni uthibitisho tosha wa juhudi za pamoja za Afrika katika mapambano dhidi ya ukatili wa albino. Unadhihirisha namna ambavyo bara limeamua kupaza sauti na kujitia kitanzi cha kuwalinda watu wenye ualbino ili wafaidi haki zao za msingi kama ilivyo kwa watu wengine.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top