Matokeo hayo yanaiweka njia panda kidogo Serengeti katika kuwania tiketi ya Madagascar, kwani wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba
Timu ya taifa ya vijana U17 ‘Serengeti Boys’ imepata ushindi wa goli 3-2 dhidi ya Congo Brazzaville kwenye uwanja wa nyumbani ikiwa ni mchezo wa kuwania kufuzu mashindano ya mataifa ya Afrika kwa vijana yatakayofanyika Madagascar mwaka 2017.
Serengeti Boys ilipata magoli yake kupitia kwa Yohana Mkomola aliyefunga magoli mawili kipindi cha kwanza huku goli la tatu likifungwa na Issa Makamba kipindi cha pili.
Congo walifunga bao lao la kwanza kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Langa-Lesse Percy baada ya beki wa Serengeti kumuangusha mchezaji wa Congo.
Serengeti ilipata pigo kipindi cha pili kufatia golikipa namba moja Ramadhani Kabwili aliyepata majera wakati akijaribu kuokoa mkwaju wa penati uliopigwa na Langa-Lesse Percy.
Benchi la ufundi la Serengeti lililazimika kufanya mabadiliko kwa kumuingiza golikipa namba mbili Kelvin Kayego ambaye alifungwa goli la pili na Bopoumela Chardon.
Endapo Serengeti itafanikiwa kuitupa nje Congo Brazzaville kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki mbili zijazo, itakuwa imefuzu kucheza michuano ya Afrika kwa vijana.