Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William LukuviWIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefuta hati tano za ardhi zilizokuwa zikimilikiwa na mfanyabiashara mwenye uraia wa Uingereza, Hamant Patel aliyemilikishwa kwa udanganyifu, huku ikiagiza watu wengine wasio raia waliomilikishwa ardhi kujisalimisha mara moja.
Aidha, wizara hiyo kupitia Ofisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Kinondoni imemuandikia notisi Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ya kulifuta shamba lake lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande, Dar es Salaam. Kauli hiyo imetolewa na Waziri William Lukuvi.
wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu uhakiki wa ofa za viwanja za Manispaa ya Jiji na Halmashauri.
Akizungumzia kuhusu kufutwa kwa hati tano zinazomilikiwa na Patel ambaye pia ni Wakala wa Kampuni ya Toyota Mwanza katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu, Lukuvi alisema wamebaini kuwa mtu huyo alimilikishwa ardhi kwa kutumia vyeti vya kughushi vinavyoonesha ni mzaliwa wa Tanzania.
Alisema hata hivyo walifanya uchunguzi na kupata taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji kuwa mtu huyo ni raia wa Uingereza na anaishi nchini kwa kutumia kibali cha Daraja la Kwanza A ambacho kinaisha mwakani.
“Nimeagiza Takukuru wafanye uchunguzi ili kubaini kama kuna maeneo mengine ambayo mtu huyu amenufaika nayo kama mzawa. Pia uchunguzi ufanyike ili kubaini wote walioshiriki hadi mtu huyu akamilikishwa ardhi,” alisema Lukuvi.
Akizungumzia kuhusu shamba la Sumaye, Lukuvi alisema shamba hilo walitoa notisi kwa kuwa halikuendelezwa kwa muda mrefu na kwamba serikali inafanya kazi bila kumuangalia mtu au cheo chake.
Ofisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Kinondoni, Rehema Mwinuka alisema tayari notisi hiyo imeshaandikwa hivyo kwa mujibu wa sheria huwa wanasubiri hadi baada ya siku 90 kisha hatua nyingine zichukuliwe.
“Kwa kawaida notisi ikishaandikwa huwa inasubiriwa hadi baada ya siku 90 kama aliyeandikiwa hakujibu basi sisi tuitafikisha mbele zaidi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua,” alifafanua Mwinuka.
Lukuvi alifafanua kuwa Ofisa Ardhi Mteule wa manispaa husika ana mamlaka ya kuandika notisi ya kufuta shamba lisiloendelezwa kwa mujibu wa sheria kabla ya kufikisha mapendekezo kwa waziri husika ambaye atamshauri Rais kufuta hati hiyo.
Katika hatua nyingine, Lukuvi ameonya kuwa amebaini kuwepo kwa baadhi ya wageni wanaoshirikiana na wazawa kufanya udanganyifu kwa ajili ya kupata miliki za ardhi.
Alisema kwa mujibu wa sheria zinaeleza kuwa ardhi ya Tanzania itamilikiwa na raia wake wenyewe na wageni wana fursa ya kupata ardhi hiyo ikiwa watahitaji kwa ajili ya uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Tunazo taarifa kuwa baadhi ya wageni wakishirikiana na raia hufanya udanganyifu na kughushi nyaraka za uraia ili kujipatia miliki za ardhi kama raia. Udanganyifu huo umekuwa pia ukifanywa na kampuni ambazo hujisajili kwa kutoa hisa nyingi kwa wazawa na baada ya kupata ardhi huhamisha hisa hizo kwenda kwa wageni,” alisema.
Alisema wameanza kazi ya uhakiki kwa kushirikiana na Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA) wa kampuni zote zinazomiliki ardhi kama raia ili kubaini kama bado zina sifa ya kumiliki ardhi kama raia au la.
Aliongeza kama itabainika kuwa kampuni hizo zimepoteza sifa ya uraia, hatua za kisheria zitachukuliwa juu ya miliki ya ardhi inayomilikiwa na kampuni hiyo ikiwemo kurejesha ardhi mikononi mwa serikali na kuwakamata wahusika.
Aidha, Lukuvi ameongeza muda wa uhakiki wa ofa za viwanja zilizotolewa na Manispaa ya Jiji au Halmashauri ili kutoa hati mpya kwa wamiliki wote wenye nyaraka hizo. Alisema hatua hiyo inatokana na utapeli unaofanywa kwa kutumia nyaraka za kughushi za barua za toleo zinazodaiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“Naagiza wananchi wote wenye nyaraka halali zilizotolewa na Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wazirejeshe kwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi. Ofisi hiyo itaweka mpango maalumu wa kuhakiki na kutoa hati miliki,” alisema Lukuvi.
Alisema kwa mtu yeyote atakayewasilisha nyaraka za aina hiyo zilizoghushiwa ataishia gerezani kwa sababu atafikishwa katika vyombo vya dola.
Lukuvi pia alisema amekuwa akipokea malalamiko mengi kuhusu uvamizi wa mashamba na viwanja vyenye hati ambapo amewaagiza Kamishna wa Ardhi na Makamishna Wasaidizi wa Kanda kuweka mkakati maalumu wa kukomesha tabia hiyo ya uvamizi kwa kushirikiana na vyombo vya dola na ofisi za halmashauri.
Post a Comment