WIZARA na taasisi za serikali, mashirika ya ndani na nje, watu binafsi na wadau wa maendeleo, wameombwa kushirikiana kuwasaidia wazee wasiojiweza na watu wenye mahitaji maalumu nchini.
Ombi hilo lilitolewa na mke wa Rais, Janeth Magufuli wakati alipokabidhi msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwenye kambi ya wazee wasiojiweza ya FungaFunga, iliyopo Manispaa ya Morogoro.
“Nichukue nafasi hii kuwasilisha kwenu salamu nyingi kutoka kwa Rais John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Janeth alisema Rais Magufuli anatambua umuhimu wa wazee kuwa ni rasilimali na hazina kubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuwa kuna mahitaji mengi katika vituo hivyo vya kuwatunza wazee na watu wenye mahitaji maalumu, dawa za kusafishia vidonda, chakula hakitoshi na wazee wanaishi kwa mlo mmoja, kambi chakavu na hatarishi na kwa ujumla hali hairidhishi.
Alisema uzee si laana bali ni mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu na kwa kutambua jambo hilo, wizara na taasisi za Serikali, mashirika ya ndani na nje, watu binafsi wenye mapenzi mema na wadau wa maendeleo washirikiane kuwasaidia wazee wasiojiweza na watu wenye mahitaji maalumu.
Alisema kwa msingi huo wa kutambua jukumu la wazee, aliona ni vyema kutoa zawadi kwao kwa kukabidhi vyakula vya aina mbalimbali ukiwemo mchele kilo 875, unga wa sembe kilo 875 , sukari kilo 175, maharagwe kilo 350 na mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi boksi moja.
Mbali na msaada wa mke wa Rais, pia wadau mbalimbali na taasisi za umma ziliungana naye kwa kukabidhi misaada ya vyakula, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood akitoa kilo 625 za sembe, Manispaa ya Morogoro kilo 500, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Morogoro kilo 40 za sukari, mafuta ya kula lita 20 na katoni moja ya sabuni.
Taasisi nyingine za umma zilizomuunga mkono mke wa Rais, ni Benki ya NMB kwa kutoa mchele kilo 50, sukari kilo 20, mafuta ya kula lita 15, chumvi na sabuni katoni moja , Benki ya CRDB mafuta ya kula lita 24, sabuni ya umma kilo 24, dawa ya meno na miswaki 36, mafuta ya kupaka kopo 24 na sukari kilo 45, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro kikichangia katoni 15 za sabuni ya kufulia.
Awali, Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Makao ya Wazee wasiojiweza FungaFunga chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii, iliyopo katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Rashid Omary alisema kambi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1970 ina uwezo wa kuhudumia wazee wasiojiweza 108 kwa wakati mmoja katika majengo mawili yaliyopo.
Post a Comment