Unknown Unknown Author
Title: Waziri Mwakyembe achachamaa TRA kuwashusha Serengeti Boys kwenye basi kisa kodi
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Waziri mwenye dhamana ya michezo Dr. Harrison Mwakyembe amekuja juu baada ya kusikia kwamba timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Se...
Waziri mwenye dhamana ya michezo Dr. Harrison Mwakyembe amekuja juu baada ya kusikia kwamba timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ilishushwa kwenye mabasi na TRA wakati ipo njiani kwenda kwa makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassani ambaye aliialika timu hiyo kwa ajili ya kupata nao chakula cha jioni.
Mwakyembe amesema ni aibu kwa taifa wakati kipindi hiki kukiwa na kampeni za kuhamasisha watanzania na wachezaji ili timu ifanye vizuri halafu wanakuja watu wengine wanarudisha nyuma jitihada zinazofanywa.
“Vijana wetu walikuwa wanakuja kwako basi lao likasimamishwa na watu wa TRA wakaondolewa kwenye mabasi magari yakachukuliwa, ikabidi viongozi wa TFF waanze kutafuta magari mengine, sijui wameingia kwenye daladala ndiyo wamewaleta hapa.”
“Nataka niseme kitu kimoja kama kiongozi wa hii Wizara, suala la kodi ni suala muhimu na ni lazima kila mtu alipe, hilo halina mbadala wala msamaha, lakini natumia fursa hii kuwasisitiza TRA kutumia busara katika kukusanya kodi.”
“Baada ya kupata hizi taarifa, namwagiza katibu wangu mkuu kukaa na katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na viongozi wa TRA wakae pamoja, haya mambo yanatia aibu. Tunakwenda kwa kiongozi wetu wan chi, wewe ndio unaona hiyo fursa kwako, nani atakupa mabilioni hayo ya fedha kwa kusimamisha magari barabarani?”
“Halafu ni kama unawatengenezea biashara kina Yono kwa sababu mwaka jana nilisoma kwenye magazeti lilichukuliwa gari la TFF, waliporudishiwa ikabidi TFF iilipe Yono milioni 20 kwa kushika lile gari. Kwa hiyo nafikiri kuna milioni sijui 30 mtalipa lakini itabidi niwaambie TAKUKURU wafatilie kama hiyo hela haiendi tena huko tena.”
“Nasema kwa masikitiko kwa sababu timu hii ilipoanza mimi nilikuwa nawafuatilia sana, mechi yao ya kwanza ilibidi wsafiri hadi Kigoma kwa basi kwa sababu accounti za TFF zilifungwa, wakafika Kigoma hoi basi lao pia likiwa hoi ikabidi waiombe timu ya Burundi kuja Kigoma kucheza nao, wakafungwa 2-1. Sasa leo basi lao linakamatwa wakati tupo kwenye kapempi ya kitaifa kuhakikisha vijana wanafanya vizuri na kuliletea sifa taifa na wewe ndio unajifanya unajua kukusanya kodi.”
“Kikishindikana hicho kikao Mh. Makamu wa Rais mimi nitakuja kushitaki kwako, sitaki kusikia tena hili deni kwa sababu ni aibu hata kusema mbele za watu kwa sababu ni sisi wenyewe ndani ya serikali tuliojichanjanya.”
Baadae usiku, ilitoka taarifa kutoka kwa afisa habari wa TFF Alfred Lucas kwamba, kampuni ya udalali ya Yono ambayo ni wakala wa TRA imetangaza kuliachia mara moja basi ambalo linatumiwa na Serengeti Boys .

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top